KUSOMA KITABU CHA ZABURI      DAY 09

| Makala

 

Zaburi 41

1  Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu.

2  Bwana atamlinda na kumhifadhi hai, Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake.

3  Bwana atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.

4  Nami nalisema, Bwana, unifadhili, Uniponye roho yangu maana nimekutenda dhambi.

5  Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea?

6  Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena.

7  Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.

8  Neno la kisirani limemgandama, Na iwapo amelala hatasimama tena.

9  Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake.

10  Lakini Wewe, Bwana, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa.

11  Kwa neno hili nimejua ya kuwa wapendezwa nami, Kwa kuwa adui yangu hasimangi kwa kunishinda.

12  Nami katika ukamilifu wangu umenitegemeza, Umeniweka mbele za uso wako milele.

13  Na atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Amina na Amina.


 

Zaburi 42

1  Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.

2  Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?

3  Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako.

4  Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.

5  Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.

6  Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.

7  Kilindi chapigia kelele kilindi kwa sauti ya maboromoko ya maji yako, Gharika zako zote na mawimbi yako yote yamepita juu yangu.

8  Mchana Bwana ataagiza fadhili zake, na usiku wimbo wake utakuwa nami, Naam, maombi kwa Mungu aliye uhai wangu.

9  Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?

10  Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?

11  Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.



 

Zaburi 43

1  Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, Uniokoe na mtu wa hila asiye haki.

2  Kwa kuwa Wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu; kwa nini umenitupa? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?

3  Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze, Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu na hata maskani yako.

4  Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu, kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu; Nitakusifu kwa kinubi, Ee MUNGU, Mungu wangu.

5  Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu.



 

Zaburi 44

1  Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale.

2  Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawaeneza wao.

3  Maana si kwa upanga wao walivyoimiliki nchi, Wala si mkono wao uliowaokoa; Bali mkono wako wa kuume, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwaridhia.

4  Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo.

5  Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao.

6  Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa.

7  Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha.

8  Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele.

9  Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala hutoki na majeshi yetu.

10  Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka.

11  Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa.

12  Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao.

13  Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.

14  Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi.

15  Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na haya ya uso wangu imenifunika,

16  Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi.

17  Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulihalifu agano lako.

18  Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako.

19  Hata utuponde katika kao la mbwa-mwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti.

20  Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu;

21  Je! Mungu hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo.

22  Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kondoo waendao kuchinjwa.

23  Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe kabisa.

24  Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu?

25  Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi.

26  Uondoke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.



 

Zaburi 45

1  Moyo wangu umefurika kwa neno jema, Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme; Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi.

2  Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu; Neema imemiminiwa midomoni mwako, Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.

3  Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari, Utukufu ni wako na fahari ni yako.

4  Katika fahari yako usitawi uendelee Kwa ajili ya kweli na upole na haki Na mkono wako wa kuume Utakufundisha mambo ya kutisha.

5  Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako; Imo mioyoni mwa adui za mfalme.

6  Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele, Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.

7  Umeipenda haki; Umeichukia dhuluma. Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta, Mafuta ya furaha kuliko wenzako.

8  Mavazi yako yote hunukia manemane Na udi na mdalasini. Katika majumba ya pembe Vinubi vimekufurahisha.

9  Binti za wafalme wamo Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki. Mkono wako wa kuume amesimama malkia Amevaa dhahabu ya Ofiri.

10  Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.

11  Naye mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.

12  Na binti Tiro analeta kipawa chake, Nao matajiri wa watu watajipendekeza kwako.

13  Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu, Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu.

14  Atapelekwa kwa mfalme Na mavazi yaliyofumwa kwa uzuri. Wanawali wenzake wanaomfuata, Watapelekwa kwako.

15  Watapelekwa kwa furaha na shangwe, Na kuingia katika nyumba ya mfalme.

16  Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako, Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.

17  Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu Katika vizazi vyote. Kwa hiyo mataifa watakushukuru Milele na milele.



 


 


 


 SADAKA